Na Lorietha Laurence-Maelezo
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeandaa kampeni kwa ajili ya ugawaji wa vyandarua vya
hati punguzo katika kaya nchini, inayotarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Wizara hiyo
Mhe.Dkt Kebwe Stephen, amesema kampeni hiyo imeanzishwa ili kuziba pengo kutokana
na kusitishwa kwa huduma ya hati punguzo iliyokuwa ikifadhiliwa na Mennonite Economic
Development Associates (MEDA) mapema mwezi Juni 2014 .
Dkt. Kebwe aliongeza kuwa jamii pamoja na wakina akinamama wajawazito watanufaika na
kampeni hiyo, ikiwemo ile ya ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi shuleni ambayo imeanza
kutekelezwa tangu mwaka 2013 kwa mikoa ya Lindi,Ruvuma na Mtwara.
“kampeni hii ni muhimu na ni mojawapo ya njia mbadala ya kuendelea kuwasaidia akinamama
wajawazito na watoto wachanga kujikinga na ugonjwa wa malaria ikiwa ni mkakati wa
kupunguza vifo vya akinamama na watoto”alisema Mhe.Dkt. Kebwe
Aidha, jumla ya vyandarua milioni 13 vimesambazwa kupitia mpango huo, ambapo imechangia
katika kuongeza matumizi ya vyandarua kwa akinamama wajawazito kutoka 16% mwaka 2004
hadi 75% mwaka 2012 na kutoka 16% hadi 76% kwa upande wa watoto.
Pia alifafanua kuwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua itaendelea kutolewa Kwa
watumiaji wa vyandarua hivyo, kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia tofauti kwa kufugia
kuku na hata wengine kuweka katika bustani ili kukinga ndege waharibifu badala ya kujikinga na
mbu.
Mpango huu wa hati punguzo ni mkakati ulioendelevu kuhakikisha kuwa makundi ya
akinamama wajawazito na watoto wachanga wanaendela kupata vyandarua ili kujikinga dhidi
ya ugonjwa wa malaria na umekuwa ukitekelezwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa
Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, Shirika la Maendeleo la
Serikali ya Watu wa Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) na Idara ya
Maendelao ya nchi ya Uingereza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...