Na John Gagarini, Bagamoyo
JIMBO la Jilin nchini China limekubali kuwekeza hapa nchini kwenye eneo la Uwekezaji la (EPZ) la Kamal lililopo Kijiji cha Kerege kwa Kikwete wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Uwekezaji huo utafanyika baada ya ujio wa baadhi ya viongozi wa Jimbo hilo kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji wilayani humo na kuonekana kuvutiwa na sehemu hiyo.

Akizungumza jana mara baada ya kutembelea maeneo kadhaa akiongozana na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza na sekretarieti ya mkoa wa Pwani na kuvutiwa na eneo hilo la uwekezaji la EPZ, Naibu Gavana wa Jimbo hilo Zhoncheng Sui alisema ameridhika na eneo hilo.

Sui alisema kuwa kutokana na urafiki wa kihistoria uliyopo kati ya Tanzania na China toka enzi za viongozi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Sung kumekuwa na ushirikiano ambao ni wa damu hivyo lazima udumishwe kwa ushirikiano wa kimaendeleo.

“Tumeona mambo mengi ambayo tunaweza kushirikiana ambapo moja ni pale kwenye eneo la uwekezaji ambapo tutakuja kuwekeza hapo kwani kuna miuondombinu mizuri ya barabara, maji na umeme pia waiteni na wenzetu waliopo hapa Tanzania ili nao waje wajionee na kuangalia namna wanavyoweka kuwekeza kwenye mkoa huu wa Pwani,” alisema Sui.

Awali akimkaribisha naibu gavana wa Jimbo hilo la Jilin mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa mkoa wa Pwani una mambo mengi ambayo wawekezaji wanaweza kuwekeza ikiwa ni pamoja na kwenye kilimo, uvuvi, utalii na mifugo.

“Fursa zipo nyingi ndani ya mkoa wetu na hata miundombinu ya barabara, anga, bandari, uememe na reli viko vizuri kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji ambao una hitaji uwepo wa mawasiliano mazuri,” alisema Mahiza.

Ujumbe huo ulikuwa na ziara ya siku moja wilayani Bagamoyo kutembelea maeneo ya uwekezaji kwenye ujenzi wa soko la kimataifa la samaki, eneo itakapojengwa bandari na eneo la uwekezaji la Kamal.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mwantumu Mahiza (katikati),Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Ahmed Kipozi (mwenye shati la kitenge) na Naibu Gavana wa Jimbo la Jilin nchini China Zongcheng Sui (pili kulia) wakiangalia bomba la maji ambalo limepasuka na kumwaga maji wakati ujumbe wa jimbo la China ulipotembelea jana eneo la uwekezaji la Kamal Kerege wilayani Bagamoyo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza akiongea na Naibu Gavana wa Jimbo la Jilin nchini China Zhongcheng Sui alipotembelea wilaya ya Bagamoyo kuangalia maeneo ya uwekezaji.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe kutoka jimbo la Jilin nchini China pamoja na watumishi wa wilaya ya Bagamoyo mara baada ya mkutano uliofanyika Oceanic Bay Hotel $ Resort mjini Bagamoyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...