MCHAKATO wa kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa CCM Zanzibar watakaowania nafasi za  Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawawakilishi (BLW) na Udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, uliofanyika jana (Agosti 01, 2015) mikoani mote.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Afisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Vuai Ali Vuai, imesema kuwa matokeo ya kinyang’anyiro hicho, yameoonyesha baadhi ya vigogo waliokuwa wakitegemewa kuibuka na ushindi wameanguka vibaya katika kura hizo za maoni zilizofanyika katika matawi mbali mbali ya majimbo yote 50 ya Zanzibar.
Vigogo walioibuka na ushindi na kuwa na nafasi nzuri  ya kuwa Wabunge au Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na waziri Kiongozi (Mst.) wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mhe. Shamsi Vuai Nahodha.

Wengine walioipita kwa nafasi ya Ubunge na Majimbo yao kwenye mabano ni Waziri wa Fedha wa SMT Mhe. Saada Mkuya, (jimbo jipya) la Welezo, Waziri wa Nchi (AR) Ikulu na Mwakilishi wa Jimbo la Dimani Mhe. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi (AR) Kazi na Utumishi wa Umma Mhe. Haroun Ali Suleiman na Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Mhe. Issa Haji Ussi Gavu,(hakuwa na mpinzani) pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa (SUKI) CCM Zanzibar Mhe. Hamad Yussuf Masauni.

Sambamba na hilo, aliyewahi kuwa Mwakilishi na Mbunge katika vipindi viwili tofauti (2000 na 2005) kupitia Jimbo la Dimani, Mkoa uliyokuwa Mjini Magharibi Unguja, Hafidh Ali Tahir, amemshinda  aliyekuwa akishikilia kiti cha Ubunge wa Jimbo hilo Abdullah Sheria na hivyo kulipiza kisasi cha kupinduliwa katika Uchaguzi wa mwaka 2010.
 
Miongoni mwa vigogo walioanguka katika mchakato huo ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Uzini, ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya NEC wa Idara ya Organaizesheni (CCM Makao Makuu) Mhe. Mohamed Seif Khatib, aliyepata kura 1,333 sawa (23.0 %) baada ya mpinzani wake Salum Mwinyi Rehani kuibuka kidedea kwa kupata kura 1,521 sawa 26.0.

Pia, Mjumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Kusini Unguja na Naibu Waziri wa Nchi za Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mahadh Juma Mahadhi, aliyepata kura 1,785.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe na Naibu Waziri wa Biashara na Masoko wa SMZ Mhe. Thuwaybah Edington Kissasi, Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya Itikadi na Uenezi Mhe. Waride Bakari Jabu (aliyeangushwa na Ibrahim Raza), Naibu Waziri wa Fedha wa SMT  Mhe. Ame Silima na Mbunge wa Jimbo la Koani sasa (Tunguu) Mhe. Amina Andrew Clement.

Katika  mchakato huo, ndani ya  majimbo mbali mbali kumejichomoza sura mpya kadhaa zinazotaka kugombea  nafasi za Ubunge na Uwakilishi katika Uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Miongoni mwao ni pamoja na Khalifa Salum Suleiman (Tunguu), Salum Mwinyi Rehani (Uzini) na Mjumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Mjini Mansuriyya Bagwanj (Chwaka) wanaogombea Ubunge, wakati  mjumbe wa NEC (W) Kaskazini “B” Mtumwa Peya, Afisa Mwandamizi wa CCM wa Idara ya SUKI (AKZ) Mohamed Ahmada Salum (Malindi), Simai Mohamed Said (Tunguu) na Yussuf Suleiman (Uzini) wanaowania Uwakilishi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hongera Saada.Uko so simple,huna makuu na unachapa kazi

    David V

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...