KUSOMA  ZAIDI  links  goes  to  sheriayakub.blogspot.com
Na  Bashir  Yakub.

Kawaida  wanandoa  wengi  wanapoingia  katika  migogoro  moja  ya  jambo  wanalokimbilia  kama  jawabu  la mgogoro  ni  talaka. 

 Kwa  misingi  ya  ndoa  za  kiislamu  talaka  huruhusiwa tofauti  na  misingi  ya  ndoa  za  kikiristo  ambazo talaka  huwa  haziruhusiwi.   

Hata  hivyo   hata  kama  ndoa  ni  ya  kikristo  ambayo hairuhusu  talaka linapokuja  suala  la  mahakama  basi  hata  ndoa  hizo  nazo  hutolewa  talaka. Ieleweke  kuwa kwa  mujibu  wa  Sheria  Ya  Ndoa ya 1971  suluhu  ya  kumaliza  utata  katika  ndoa  si  talaka  tu. 

Na hii ni kutokana  na  umuhimu  wa  ndoa.  Katika  hili sheria ya  ndoa imetoa  chagua  jingine  ambalo  mtu  anaweza  kulitumia  kama  mbadala  wa  talaka. Hili  linahusu  kutengana  kama  tutakavyoona.

1.KUTENGANA  KISHERIA.
Kutengana   kwa  mujibu  wa  sheria  ni  hatua ambapo  watu  wawili  mwanamke  na  mwanaume  walio  katika  ndoa halali  huamua kutoshirikiana  katika  mambo kadhaa ya  kindoa  huku  ndoa  ikihesabika kuwa  haijavunjika. Katika  hili kinachositishwa ni baadhi ya  haki  na  wajibu  wa  kindoa. Lakini kusitishwa  kwa  wajibu  na  haki    hizo  hakuhesabiki kuwa  kumevunja  ndoa.

2.   AINA  ZA  KUTENGANA  KISHERIA.
Kisheria  zipo  njia  mbili  ambazo  wanandoa  wanaweza  kutumia  ili   kutengana.  Kwanza   ni kuwa  wanandoa wanaweza  kutengana  wenyewe  kwa  hiari  yao .  Kutengana  kwa  hiari  ni  kuwa  wanakubaliana  kutengana  kwa  muda fulani  kutokana  na  kutoelewana  kwasababu  mbalimbali  za kifamilia.
Pili wanaweza  kutengana  kwa  kutenganishwa  na  mahakama kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  99  cha sheria  ya  ndoa  1971. Hii  ni  baada  ya  mmoja  wa  wanandoa  kuiomba  mahakama  iwatenganishe  kwa  kipindi  fulani  na  mahakama  kuridhika  kuwa  ipo  haja  hiyo. Mara  nyingi  kutengana kwa njia  ya  mahakama  hutokea  baada  ya  hatua  za  kutengana  kwa  hiari  kushindikana.  Mara  kadhaa    hutokea  ambapo mmoja wa  ndoa   huwa  amekerwa  na baadhi  ya  tabia  na  hivyo  kumuomba  mwenzake  watengane  ambapo   mwenzake  hukataa.  Inapotokea  hivyo  ndipo  mwanandoa  anapolazimika  kukimbilia  mahakamani  kuomba   kutengana.

3. TOFAUTI  YA  KUTENGANA  NA  TALAKA.
Talaka  ni  hatua  ambapo   ndoa  hutangazwa  kuwa  imevunjika  kabisa  na  kila  mmoja hutakiwa kuendelea  na maisha  yake. Talaka    huambatana  na  haki  ikiwemo  ile  ya  mgawanyo  wa  mali.  Wakati  kutengana  ni  hatua  ya  kuchana  kwa  muda  na  kurudiana  baadae. Kutengana  hakuambatani  na  haki  ya  kugawana  mali  za  machumo  ya  wanandoa.

4.  UMUHIMU  WA  KUTENGANA BILA  TALAKA.
Sheria  imeelekeza  tendo  hili  la  kutengana  kwa  kuzingatia  maslahi  mapana  ya  wanandoa,  familia  na  jamii  kwa  ujumla. Lengo  kuu  la  hatua  ya  kutengana  ni  kutoa  nafasi  kwa  walengwa  wanandoa  kujirekebisha . Inaaminika  kuwa  katika  kipindi  ambacho  wanandoa  hutengana   huwa  kuna  mwanya  mkubwa  ambao  hupelekea  kurekebisha  baadhi  ya tabia  ambazo  zilikuwa  kikwazo. Kutengana ni nafasi ya    mtu  kujirudi.

5.  MATUNZO  YA  MWANAMKE  NA  WATOTO  KIPINDI  CHA  KUTENGANA.
Kwa  upande  wa  mwanaume  ni  lazima  kwake  kuendelea  kutoa  matunzo  ya  mwanamke pamoja  na ya watoto kama  wapo. Kisheria  mwanaume  ndiye  huwajibika  kutoa matumizi  ya  watoto  pamoja  na  kumtunza  mke wake. Katika  kipindi  cha  kutengana  haki  na  wajibu  huu  huendelea mpaka  kipindi  cha  kutengana  kitakapoisha. Hata  hivyo  yapo  mazingira  ambapo  mwanamke  anaweza  kutakiwa  kutoa  matunzo  kwa  mwanaume kama  itakavyokubaliwa katika  masharti  ya  kutengana.

6.  MUDA  WA  KUTENGANA.
Kawaida (practice) muda  wa  kutengana  unaotakiwa  inabidi  iwe  miaka   miwili  na  ikizidi  isizidi  mitatu. Ikiwa  muda  huo  utapita  bila  muafaka  kwa  wahusika basi  hatua  za  talaka  zinaweza  kufuata.

7.  KUAMUA KUSITISHA MUDA  WA  KUTENGANA.
Kifungu  cha  113 ( 1 ) kinatoa  uhuru  kwa wanandoa  kutuma  maombi  ya  pamoja  mahakamani  kuomba  kusitishwa  kwa  amri  ya  kutengana. Hii  ni  ikiwa  kutengana  kulitokana  na  amri  ya mahakama.  Ikiwa kutengana  hukukutokana  na  mahakama  ila  ilikuwa  kwa  ridhaa  ya  wanandoa basi  wahusika  kwa  hiari  yao  wanaweza   kuamua  kusitisha  bila  kuhitaji  amri  ya  mahakama.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kwa mujibMara nyingi huwa wanadoa wanatengana bila hiari yao wenyewe,pia bilakutenganishwa na mahakama.Kinachotokea hapo huwa mwanadoa mmoja anashindwa kuvumilia tabia za mwenzake,ama makwazo ya mwenzake na kuamua kujitenga mwenyewe na kumuacha mwenzake. Je hilo linakaaje kwa mujibu wa sheria hii?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...