Kutoka Kushoto - Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio,  Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Nishati na Madini (Uganda), Dkt. Fred Kabagambe Kaliisa na Meneja Mkuu wa Total E&P Uganda, Ndg. Adewale Fayemi wakipongezana baada ya kutia saini Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya Serikali ya Uganda na Tanzania juu ya utekelezaji wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda (Kabaale) mpaka bandari ya Tanga (Tanzania). 

 SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA (TPDC)


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda, TPDC na Total E&P Uganda wametia saini Hati ya Makubaliano juu ya utekelezaji wa mradi wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda kupitia Tanzania.

Hati hii ya Makubaliano inafungua fursa kwa Serikali hizi mbili kufanya kazi kwa pamoja kuangalia uwezekano wa kuendeleza mradi wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale Uganda kupitia Tanzania mpaka bandari ya Tanga. Makubaliano haya pia yanatambua faida zaidi zitakazopatikana kwa Tanzania na Uganda ambazo ni zaidi ya utekelezaji wa mradi huu. Vilevile makubaliano haya yanatoa muongozo kwa pande zote zinazohusika kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kuboresha tafiti zilizo kwisha fanyika juu ya njia ya Tanga.

Akiongea baada ya kusaini hati hiyo, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava alisema “Tanzania na Uganda wana historia ndefu ya ushirikiano na mradi huu utazidi kuboresha ushirika kati ya nchi hizi”. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio aliongeza kuwa, TPDC ina uzoefu wa muda mrefu katika ujenzi, uendeshaji na utunzaji wa bomba na hivyo uzoefu huu utasaidia sana katika utekelezaji wa mradi huu. Wiki hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifungua rasmi mradi wa bomba la gesi la kilometa 542 kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam unaomilikiwa na kuendeshwa na TPDC.

Imetolewa na;
Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,
S.L.P 2774,
Dar-es-Salaam.
Tanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...