Kwa kifupi Shirika limeitikia wito
wa Serikali wa kuhakikisha mashirika yanayopokea ruzuku toka Serikalini
yanajijengea uwezo wa kujitegemea kwa kupunguza utegemezi serikalini. Pia
mashirika ya aina hiyo yanawajibika kuendesha tafiti na kuendeleza teknolojia
za gharama nafuu zinazolengwa kuwasaidia watanzania kujijengea uwezo wa
kujikwamua kiuchumi.
Katika kipindi cha miaka 10 ya Serikali ya awamu ya nne
Shirika la Mzinga limefanya yafuatayo:-
1. Uzalishaji wa Baruti
Shirika
limezalisha baruti na kuanzisha vituo vya uuzaji wa baruti hizo katika maeneo
ya Mererani (Simanjiro), Arusha, Shinyanga na Mpanda kwa lengo la
kuwarahisishia wachimbaji wadogo kupata nyenzo hiyo inayowasaidia katika
shughuli za uchimbaji madini badala ya kuwaachia wachimbaji wakubwa uwezo huo
peke yao. Usafirishaji wa baruti ni hatari kubwa kwa maisha, na sheria inazuia
wachimbaji wadogo kufanya hivyo kwa ajili ya usalama wa maisha yao. Shirika
linawafikishia nyenzo hiyo huko waliko, na juhudi za kufikisha nyenzo hiyo
kwenye maeneo mengine zinakofanyika shughuli za uchimbaji zinafanyika.
2. Utengenezaji Samani
Shirika
limeitikia wito wa Serikali wa kuzalisha samani imara zinazotokana na mbao
ngumu nchini kwa ajili ya matumizi serikalini kwa lengo la kupunguza na
hatimaye kuondoa matumizi ya samani dhaifu zinazotengenezwa nchi za nje. Samani
hizo za nje zinaligharimu taifa fedha nyingi lakini hazidumu ikilinganishwa na
samani zinazozalishwa hivi sasa na Shirika la Mzinga kwa kutumia mbao halisi.
Shirika limewekeza katika teknolojia ya kisasa katika kutekeleza jukumu hili.
3. Mashine za kuchakata mazao
Shirika
limejikita pia katika kuzalisha mashine mbalimbali za kuchakata mazao zikiwemo
mashine za kukoboa na kusaga chakula cha binadamu, mashine za kusaga na
kuchanganya chakula cha mifugo, mashine za kukamua alizeti, na nyingine nyingi.
Kote zilikouzwa, mashine hizo zimetengeza ajira za moja kwa moja na zisizo za
moja kwa moja kwa watu na vikundi vinavyoshiriki kuzifanya mashine hizo kuzalisha.
Changamoto kubwa katika eneo hili ni uwezo mdogo wa wananchi kununua mashine
hizo. Shirika linawashauri wananchi kujiunga katika vikundi na kuwasiliana na
Shirika juu ya namna bora ya kujipatia mikopo kutoka katika mabenki itakayowawezesha
kununua teknolojia hizo.
4. Shughuli za ujenzi
Mwaka
2012 Shirika lilianzisha kampuni tanzu ya ujenzi (Mzinga Holdings) ambayo
katika kipindi cha miaka mitatu imeweza kupewa na kukamilisha miradi mingi kwa
lengo la kulipunguzia Shirika mama utegemezi kwenye ruzuku toka serikalini.
Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa soko la Kemondo, (mkoani Kagera),
Ujenzi wa hostel ya Masista wa St. Theresa (Kashozi, Kagera), Ujenzi wa kiwanda
cha maji cha Bunena (Bukoba), Ujenzi wa daraja la Mabwepande (Dar es Salaam),
Ujenzi na ukarabati wa majengo ‘Air Force Station’ (AFS, Mwanza), ukarabati wa
nyumba 40 za Jeshi huko Kitangiri (Mwanza), ujenzi wa nyumba za halmashauri za
Masasi na Morogoro, ujenzi wa hospitali ya wilaya (Mkundi, Morogoro) na ujenzi
wa mazingira na uwekaji samani kwenye makao ya kudumu ya Chuo cha Ukamanda na
Unadhimu (Tengeru, Arusha).
5. Utafiti
Shirika
linashirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti katika kuendesha tafiti na
kutengeneza vifaa vinavyotokana na tafiti hizo. Baadhi ya taasisi hizo ni
pamoja na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, na Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH), CoET, CAMARTEC,
TIRDO
n.k.
Kwa maelezo ya kina ona
powerpoint presentation ifuatayo:
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...