JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametembelea kwa ghafla wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam, na kujionea hali ya msongamano mkubwa wa wazazi uliosababishwa na uhaba wa vitanda na nafasi finyu katika wodi hiyo.

Rais Magufuli aliyekuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumuona na kumjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Bin Ally, amelazimika kwenda katika wodi hiyo baada ya msafara wake kusimamishwa na kundi la akina mama, waliomtaka kwenda katika wodi ya wazazi ili akajionee jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.

Baada ya kujionea mwenyewe kero ya msongamano na kuzungumza na baadhi wazazi waliojifungua, Rais Magufuli amewaahidi wazazi hao kuwa atashughulikia kero alizozishuhudia.

"Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso, na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua" alisema Rais Magufuli.

Kabla ya kutembelea wodi ya wazazi, Dkt. Magufuli amemjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Ally aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo amempa pole na kumuombea apone haraka.

Pamoja na kupokea pole ya Rais, Mufti wa Tanzania ameongoza dua ya kumuombea heri Rais Magufuli ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake katika kuwahudumia watanzania.

Dua kama hiyo pia imefanywa na wananchi wengine waliokuwa wakimsubiri nje ya majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo katika dua hiyo wamemuomba Mwenyezi Mungu kumlinda na kumuongoza katika majukumu yake ya kuiongoza nchi.

"Mwenyezi Mungu mbariki Rais wetu, mpe hekima, busara na upendo katika kazi zake za kuiongoza nchi hii ili watanzania wote wanufaike" ilisema sehemu ya dua hiyo iliyoongozwa na mmoja wa akina Mama.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
10 Februari, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimjulia hali Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir akimuombea Dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mara baada ya Rais Dkt. Magufuli kumjulia hali Hospitalini hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiombewa Dua na ndugu na jamaa mbalimbali ambao walifika Muhimbili kuwaona wagonjwa wao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akielekea katika Wodi ya Wazazi kufanya ukaguzi wa ghafla mara baada ya kuwasili akitokea Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wagonjwa waliolazwa katika Wodi ya Wazazi na amewaahidi kutatua kero zao ndani ya muda mfupi ujao. PICHA NA IKULU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Nashauri wanaohusika na mavazi ya Mhe Rais, hii tshirt ya ndani haiendani kabisa na hadhi yake. bora angevaa nyeupe, lakini ukishavaa koti tshirt hiyo haitakiwi. Please muonekano wa Rias wetu ni muhimu sana.

    ReplyDelete
  2. Afadhali mtowa maoni wa mwanzo hapo juu umeweza kuliona hilo, khususan hali ya hewa pia wakati mwingine ikiwa ya joto sana, basi kwa mvao huo mara mwili unaanza kuchonyota kwa joto na mara ukitahamaki ushaanza kujisasambuwa moja moja upate takhfif. Lakini uzuri wa Mh. Rais wetu hana makuu, ispokuwa tu linalowezekana kurekebishwa katika mavazi yake, basi wahusika wajitahidi ili mavazi yaendane na hadhi, muonekano pamoja na mazingira yake husika.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...