Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo akiongozana na baadhi ya viongozi wa makampuni ya mafuta wakati wa ziara ya kukagua matanki ya kuhifadhia mafuta leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo akiongea na baadhi ya viongozi wa makampuni ya mafuta wakati wa ziara ya kukagua matanki ya kuhifadhia mafuta leo jijini Dar es salaam ili kujionea hali ya upatikanaji wa mafuta ya ndege baada ya kugundulika baadhi ya shehena ya mafuta hayo yaliyoingizwa nchini yalikuwa yamechanganyika na mafuta ya petroli. Kwa picha zaidi BOFYA HAPA |
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Serikali imewatoa
hofu na kuwahakikishia Watanzania na abiria wanaotumia usafiri wa anga nchini
kwamba mafuta ya ndege yapo ya kutosheleza matumizi kwa muda wa siku 14 wakati
shehena nyingine za mafuta hayo zinaendelea kuingia nchini.
Hayo yamesememwa na
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alipofanya ziara leo jijini
Dar es salaam kukagua matanki ya kuhifadhia mafuta ili kujionea hali ya
upatikanaji wa mafuta ya ndege nchini baada ya kugundua baadhi ya shehena ya
mafuta hayo yaliyoingizwa nchini yalikuwa yamechanganyika na mafuta ya petroli.
“Mafuta ya ndege yapo
na ndege zitaendelea kufanya safari kama ratiba zao zilivyopangwa na Watanzania
msiwe na wasiwasi, tumejiridhisha, mafuta yanatosheleza kwa muda wa siku 14
wakati hatua ya shehena nyingine kuingia nchini zinaendelea” alisema Prof.
Muhongo.
Ziara hiyo ya Waziri Prof.
Muhongo inafuatia kugundulika kwa mafuta ya ndege yaliyoingizwa nchini mapema
mwezi Mei mwaka huu, ambayo hayafai kwa matumizi yaliyokusudiwa kutokana na kuchanganywa
na mafuta ya petroli.
Aidha, Prof. Muhongo
ameitaka kampuni ya Sahara Energy Resources yenye makao yake makuu nchini
Nigeria ambayo ndio ilioingiza mafuta hayo nchini, kusimamisha shughuli zake
mara moja hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Imeonekana si mara ya
kwanza kwa kampuni hiyo kuingiza mafuta machafu nchini, hatua iliyomfanya
Waziri huyo kuchukua msimamo huo wa Serikali hadi suala hilo litakapopatiwa
ufumbuzi.
Akizungumzia hatua
hiyo na hali ya mafuta nchini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Uingizaji
Mafuta kwa Pamoja nchini, Michael Mjinja amesema kuwa mafuta ya ndege yapo na yanatosheleza
kwa wiki mbili kuanzia sasa.
Mjinja aliongeza kuwa
wanakuhakikisha uhaba wa mafuta hayo hautokei tena nchini ambapo wanaendelea
kushirikiana na kampuni ya Total na SP Rwanda ambazo hadi sasa ndio zenye
mafuta safi yanayokubalika kwa matumizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya TIPER iliyoko eneo la Kigamboni jijini Dar es salaam,
Stephane Gay amesema kuwa kampuni yake ina nafasi ya kutosha ya kuyahifadhi
mafuta yote ambayo hayastahili kutumika ili matanki na mitambo ya kampuni zote
zilizopata mafuta hayo yafanyiwe usafi upya tayari kwa kuweka mafuta safi
yanayoingia nchini.
Ziara ya Waziri Prof.
Muhongo imehusisha kutembelea matanki ya kampuni tano za mafuta ikiwemo Puma,
GAPCO, Oil Com, TIPER pamoja na Kampuni ya Oryx Energies.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...