Na Benedict Liwenga-WHUSM.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameahidi kuzitataua baadhi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) ikiwemo upatikanaji wa Hati Miliki ya Kiwanja kwa ajili ya kazi zao, Ushuru unaotozwa kupitia Idara ya Maliasili nchini pamoja na Sheria ya Tozo katika Viwanja vya Ndege.

Mhe, Nnuaye ametoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Wanachama wa Shirikisho hilo ambapo amesema kuwa, suala la upatikanaji wa Hati Miliki ya eneo kwa ajili ya kazi za Wachongaji hao alishaanza kuifanyia kazi kwa kufanya mawasiliano na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na amewahakikishia kwamba Hati ya eneo hilo itapatikana ili Wachongaji hao waweze kuwa na eneo lao maalum la kazi zao.

‘’Suala la upatikanaji wa Hati Miliki katika eneo lenu ambalo limekuwa likileta minong’ono niachieni mimi kwani najua katika hili kuna baadhi ya watu wenye fedha wanataka kuwakandamiza watu wasio na uwezo kwa kudai kuwa eneo ni la kwao, hapo awali nilishafanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na nawahahakikishieni kuwa haki itatendeka, kwani hakuna mtu mwenye mfuko mkubwa wa kuweza kuiingiza Serikali nzima katika suala hili’’, alisema, Mhe. Nnauye.

Kuhusu suala la Ushuru unaotozwa na Maliasili nchini, Mhe. Nnauye amesema kuwa yuko tayari kukaa na watu wa Maliasili na kuona namna gani ushuru huo unavyotozwa hususani kwa Wachonagji hao pasipo kuonewa mtu ambapo pia ameshauri kuwa baadhi ya kodi ambazo zinazoweza kuua biashara za watu wenye vipato vya chini ni vema zikaondolewa ili zisiendelee kuwaumiza.

Aidha, Mhe, Nnauye ameahidi kutembelea maeneo ya Viwanja vya ndege ili kuweza kujua baadhi ya bidhaa za kazi za Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa na Watendaji viwanjani hapo zimekuwa zikiishia wapi ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa katika viwanja hivyo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akipokea maelezo kuhusu sanamu iliyochongwa toka kwa Mwandamizi na Msemaji wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) Bw. Nyunga Joseph Nyunga wakati alipotembela katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (wa tatu kushoto) akiangalia kazi za sanaa ya uchongaji ndani ya moja ya mabadanda ya Wachongaji hao wakati alipotembela katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (katikati) akiwa ameongozana na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) wakati alipowasili katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.

PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...