Kesi dhidi ya mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein
maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng'ombe imeamliwa kuendelea kusikilizwa
baada ya mshtakiwa huyo kukana baadhi ya maelezo ya awali (PH), licha ya
mwanzoni mwa wiki hii kukubali shtaka la utakatishaji wa fedha kiasi cha USD
540,000.
Mapema wiki hii, Ndama alikiri kutenda kosa hilo
ambalo ni kosa la sita kati ya anayoshtakiwa nayo, na mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu ikapanga leo iwe siku ya kusomewa maelezo ya awali (PH), kabla ya
kumsomea hukumu yake.
Hata hivyo, wakati akisomwa Maelezo hayo na wakili
wa serikali Christopher Msigwa Ndama alikana baadhi ya tuhuma na kukiri chache
kitendo kilichofanya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa kuamuru
kesi hiyo iendelee kama kawaida kwani tuhuma alizokataa mshtakiwa ndizo
zinajenga msingi wa kesi.
Ndama anayetetewa na Wakili Jeremiah Mtobesya alikiri
baadhi ya maelezo ya awali aliyosomewa na wakili wa Serikali Msigwa ikiwamo
nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika kuingizwa hizo fedha, hundi
zilizotumika kutolea hizo fedha, maelezo ya benki ‘bank statement’ na Swift
massage.
Hata hivyo alikana baadhi ya maelezo ambayo ni
sehemu ya kuunda shtaka hilo, na kusema kuwa hawajui wakurugenzi wa kampuni ya
Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited wanaotambulika Brela,
Bushoboka Mutamura na Mujibu Hamis Taratibu.
Aidha alikanusha kuwa kampuni ya Muru Platnum
Tanzania Investment Company Limited haikuwahi kuingia mkataba na Australia kwa
kampuni ya Trade TJL DTYL Limited na kwamba hakuwahi kuwagaia wabia
wenzake fedha hizo taslimu kwa lengo la kuficha chanzo chake.
Baada ya mshtakiwa kukana baadhi ya PH Msigwa alidai
mahakamani hapo kuwa kwa kuwa mshtakiwa alikuwa amekiri kosa ni rahisi
kuthibitisha yaliyofanyika na kwamba kwa kadiri maelezo ya awali yalivyosomwa na
majibu ya mshtakiwa basi ni jukumu la mahakama kuangalia kama maelezo aliyokubali
yanakidhi kumtia hatiani ama kesi ianze kusikilizwa.
“Ili haki ionekane imetendeka na kwa vile mshtakiwa
anakubali baadhi ya maelezo na mengine ameyakataa mahakama inaona ni vema kesi
ianze kusikilizwa ili kila upande upate haki yake kwani mshtakiwa alitakiwa
akubali shtaka hili bila ya kupinga lakini kwa kuwa amekana baadhi ya tuhuma ni
wazi kuwa amekana shtaka”, amesema Hakimu Nongwa.
Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, Msigwa ameiambia
mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kesi itatajwa tena Juni
6, mwaka huu.
Mei 16, 2017, Ndama alikubali shtaka la sita la
kutakatisha fedha ambapo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014,
Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum
Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye benki
ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani
540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la
kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mashtaka mengine anayokabiliwa nayo ni kughushi na
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...